Baada ya takriban miaka minne ya uadui mkubwa, Lady Jaydee ametangaza kuwa hana tatizo tena na Clouds Media Group. Uamuzi huo umekuja baada ya Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kudai kuwa wapo tayari kuanza kucheza nyimbo za muimbaji huyo mkongwe iwapo atawapa ruhusa.
Kujibu ofa hiyo, Jaydee alisema kauli ya Ruge ni ni sahihi na ya kiutuzima.
Muimbaji huyo mkongwe alitoa kauli hiyo kwenye mahojiano na mtangazaji wa Nyemo FM, ya Dodoma, Winston Makangale. “Nimeisikia kauli ya Ruge, kwa namna aliyoiongea na nafasi aliyokuwa nayo, sioni kama kuna kitu kibaya chochote alichokifanya kwa jinsi ambavyo amezungumza, naona amezungumza sahihi tu,” alisema.
“Hajanipigia simu na wala sijampigia simu, kwahiyo sio kwamba tumeongea kitu chochote lakini nayaona tu ni maamuzi ya kikubwa ambayo yamefanyika hapo. Hatujaongea kwasababu tulikuwa na mgogoro,” ameongeza.
Jaydee alisema uongozi wake ndio utakaokuja na maamuzi kufuatia ofa ya Ruge. “Kama kuna kauli yoyote ambayo itatakiwa kutoka, management itatoa kauli hiyo ya nini kitafuata.”
Na Jumatano hii kupitia kipindi cha Amplifaya cha Clouds FM, uongozi wa Lady Jaydee ulitoa taarifa yake rasmi kuhusiana na kuwa tayari kufanya kazi tena na kituo hicho.
“Hatuna tatizo na Clouds Media Group kuanza kupiga nyimbo za Lady Jaydee. Wanaweza kuanza kupiga wakati wowote watakapokuwa tayari kwakuwa chochote kilichotokea hapo nyuma kimefikia tamati, la msingi sasa ni amani na upendo vitawale,” yalisema maelezo yake.
“Kuanzia leo wana uhuru wa kupiga na kutaja jina la Lady Jaydee kadri wawezavyo.”
Wiki iliyopita kwenye mahojiano na kipindi cha XXL, Ruge alisema: Tatizo ni kwamba hakuna ambacho hatujamaliza, tulimaliza, tunasubiri order. Unajua kimsingi ulipopewa order ya kwamba ‘nyimbo zangu usipige, jina langu usiseme kwenye chombo chako, vyovyote itakavyokuwa mimi sitaki kusikia hiyo kitu’ hiyo ndio order. Kwahiyo labda tukikutana, nimuombe tena [Lady Jaydee] kama tutaruhusiwa kufanya hiyo kitu.”
Wiki kadhaa zilizopita Ruge na Joseph Kusaga walishinda kesi ya kuchafuliwa (defamation) iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Lady Jaydee na muimbaji huyo kuamriwa kuwaomba radhi.
“Tunashukuru walau tulishinda ile kesi lakini at least ilitengeneza mfano wa watu kuelewa kwamba tusipende kutuhumu vitu kama watu huna uhakika. Bahati nzuri pia hata katika hiyo kesi alisema mwenyewe hajawahi kusikia tunasema, aliambiwa na watu. Lakini ni mambo yashapita hayo.”