Darassa ni hadithi ya mafanikio ambayo kila mdau wa muziki ataikumbuka kwa mwaka 2016. Na hadithi yake ina funzo kubwa katika namna ambayo hit song hupatikana. Pengine nilichojifunza zaidi ni kuwa hakuna formula ya jinsi ya kupata hit.
Kwamba ‘don’t bother, just hit the studio do what you love’ mengine yatajulikana mbele ya safari, right? Kwasababu wakati mwingine ule wimbo ambao msanii aliurekodi kwa kujiachia tu studio kuwapa mashabiki wake zawadi, hugeuka kuwa mkubwa hadi humshangaza yeye mwenyewe. Na wakati mwingine, wimbo ambao msanii huuwekea mikakati mikubwa, kufanya uwezekaji wa kufa mtu na promo nzito, hugeuka kuwa ‘flop’ na ‘disappointment’ kubwa.
Kilichotokea mwaka huu kwa Darassa ni mawimbi ambayo kila kona imeyahisi. Muziki umegeuka kuwa wimbo wa hadhi ya ‘national anthem’ kwa muda mfupi. Ndio wimbo wenye rotation kubwa zaidi nchini kwa sasa. Huwezi kuukwepa. Usipousikiliza kwenye redio, utaona video yake kwenye TV. Usipousikia kwenye baa ya jirani, utausikia kwenye bajaj au bodaboda inayokatiza wakati ukitembea barabarani. Kwa ufupi katika mzunguko wako saa 12 za siku, uhakika wa sikio lako kuguswa na mawimbi ya mdundo wake ni mkubwa, utake ustake au labda uweke pamba sikioni.
Na kwa muda mfupi, Darassa amegeuka kuwa msanii wa rap mwenye show nyingi. Darassa amegeuka ‘hot cake.’ Hivyo inamlazimu kusafiri muda mwingi kwaajili ya kutumbuiza. Mfano siku kadhaa zilizopita alikuwa na show tatu katika mikoa miwili tofauti, Iringa na Shinyanga. Ni katika safari yake ya kutoka Kahama kwenda Kakola mkoani Shinyanga ndipo yeye na timu yake walipopata ajali ambayo kama si rehema za Mungu, angegeuka kuwa #hashtag.
Katika wakati huu ambao Darassa anafanya vizuri, amekuwa akipata ushauri mwingi kutoka kwa watu wanaotaka afike mbalimbali zaidi na kwamba asije siku moja akapotea tena baada ya kufika kwenye kilele cha mafanikio kimuziki. Hofu hiyo haikwepeki sababu kuna mifano mingi ya watu waliowahi kutoa nyimbo za ukubwa huo lakini leo hii wanapumulia mashine.
Miongoni mwa ushauri anaoupata ni kuwa apunguze show anazofanya kwa kuweka dau kubwa zaidi ili kuzichuja. Moja ya waliompa ushauri wa aina hiyo ni Sebastian Ndege, ambaye katika sehemu ya alichomshauri anasema, “Usichukue show za mapromoter uchwara waka dissapoint mashabiki wako kuwatia hasira na kukushusha hadhi. Bora ufanye shows chache lakini za ukweli, with detailed showcase.”
Mwingine ni Le Mutuz ambaye anamshauri kuwa ni muda wa yeye kuanza kuchukua malipo ya shilingi milioni 15 hadi 20. Na pia kuwapa masharti mapromota wa maeneo ya mbali kumtafutia usafiri wa ndege. Kwa upendo, wote, wametoa ushauri unaoweza kumjenga japo mwingine unakuwa ni nje ya uhalisia.
Nakubali kuwa kutokana na alipofika, Darassa hapaswi kulipwa kiasi kile kile kama ambacho alikuwa anatoza miaka miwili iliyopita, lakini hilo linapaswa kwenda kwa process. Ni haraka mno kutoka kulipwa mfano milioni 4 kwa show hadi kuwa milioni 20. Inahitaji justification zaidi ya kuwa na hits mbili kuweza kulipwa kwa ukubwa huo.
Watu wasimjaze maneno Darassa na kuanza ajisikie kuwa anapaswa kuanza kuchukua kiasi kile kile ambacho wasanii kama Diamond au Alikiba wanachukua – kumbuka safari ya wawili hawa na nguvu waliyojikusanyia hadi sasa. Hapo alipofika Darassa, kuna rappers kibao nyuma waliwahi kufika, lakini hawakulazimisha kupaa juu ghafla na kutaka walipwe mamilioni ya shilingi ambayo hayaendani na uhalisia.
Huu ndio muda ambao Darassa anaendelea kujijenga kujitengenezea ukubwa huo wa kutoza fedha nyingi au kuzikataa zile zinazoitwa ‘show za vichochoroni.’ Kumbuka kabla ya kuachia Muziki, hakuwa na ‘demand’ hiyo ya hata kuitwa kwenye utitiri wa show hizo. Show za milioni 3, 4 ndizo zinaweza kumjengea na kumtengenezea mazingira ya kudai shilingi milioni 15 au 20 kwa show moja baadaye. Hizi ni show zinazompa mtaji wa kujitengenezea himaya yenye nguvu itakayompa kiburi ya kukataa milioni 5 ili alipwe milioni 15.
Kuna wasanii wanaofanya vizuri ambao kupata show ya milioni 2 au 3 ni ngekewa, haiwezakani Darassa kuzikataa kisa ametoa hit ndani ya mwezi mmoja. Isitoshe, show za vichochoroni ndizo zinaonesha ukubwa wa msanii na dalili kuwa muziki wake umefika mbali. Ehh, ndiyo, haiwezekani kujiita msanii mkubwa wakati unajulikana mjini tu.
Ushauri wangu kwa Darassa ni kwamba aendelee kuwa mnyenyekevu hivyo hivyo kama alivyo sasa bila kuanza kuweka attitude kuwa hataki kwenda baadhi ya sehemu ambazo hazifikiki kwa ndege. Wanasema Roma haikujengwa kwa siku moja, ama hata mbuyu ulianza kama mchicha.. Ni process, inahitaji muda kutengeneza ukubwa, hauji ndani ya siku moja.