Wasanii wote wakubwa wa zamani walikuwa wachanaji. Hits zote za zamani zilifanywa na wasanii wa hip hop. Watu wa kwanza kulipwa fedha za show, walikuwa watemaji wa rhymes.
Waimbaji waliofanikiwa miaka hiyo wengi walikuwa wanawake, wakiwemo Lady Jaydee, Ray C, na Stara Thomas. Mambo yalikuja kubadilika tu miaka kama mitano iliyopita, na waimbaji wakaibuka kuwa wasanii wakubwa kiasi cha kuvuka zaidi border.
Upepo huo ndio uliosababisha kuwepo majina makubwa sasa ya wasanii kama Diamond, Alikiba, Vanessa Mdee, Ben Pol, Ommy Dimpoz, Rich Mavoko, Navy Kenzo na wengine. Pia kizazi cha miaka ya hivi karibuni kama vile Raymond, Harmonize, Barakah The Prince na wengine.
Ukafika muda, wasanii wa kuimba wakateka agenda katika mazungumzo ya kila siku ya muziki wa Bongo Flava. Hiyo ilisababishwa na uthubutu wao katika kuwekeza fedha nyingi kwenye kazi zao ikiwemo kufanya video kubwa. Hiyo ndio sababu wasanii wa kuimba wakawa kitovu cha mazungumzo kwenye vyombo vya habari, mtaani na kwenye mitandao ya kijamii.
Lakini mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu rappers wameonekana kutaka kurudisha ubabe wao. Ni wazi kuwa rap sasa imetawala zaidi agenda za muziki wa Tanzania. Hits nyingi sasa hivi ni za wasanii wanaorap. Ukianza na anthem ya Darassa, Muziki, ambayo imemweka kwenye daraja la aina yake kwenye rap ya Bongo, hits kama Dume Suruali ya FA, Roho ya Fid Q, Pesa ya Madafu, Perfect Combo ya Joh Makini, ziliufunga mwaka 2016 kwa kishindo.
Na ukiangalia hits nyingi kwenye rotation ya muziki sasa, ni za wasanii wanaorap. Ngoma kama Umeniweza ya The Amazing, Sijiwezi ya Nay wa Mitego, Hela ya Madee, Mazoea ya Bill Nas na Mwana FA, Sinaga Swagga ya Young Killer, Usimsahau Mchizi ya Roma na Moni na zingine zinafanya vizuri kuzidi ngoma kibao za wasanii wa kuimba.
Collabo za kimataifa kama ile ya AY na Nyashinski, More and More na zingine zinazosubiriwa kuja ikiwemo ya Young Killer na Khaligraph, zinarudisha heshima ya rap Tanzania. Na ukiangalia video za ngoma hizo, utagundua kuwa rappers hawataki tena ubahili kwenye kazi zao kama walivyokuwa mwanzo.
Mabishano na majigambo ya wasanii wa Bongo kwa sasa yametawaliwa zaidi na rappers na hata vituo vya redio vimeonesha kuicheza zaidi ngoma yao. Mistari tata kama ya Young Killer dhidi ya Joh Makini, Young Dee na Dogo Janja au ile ya Madee dhidi ya Nay wa Mitego, imezalisha mijadala mirefu na kuipa favor rap.
Nadhani hamasa kama hiyo ilikuwa ikihitajika zaidi kwa sasa kwenye muziki wa Bongo ili kuwapa chaji wasanii wa rap waliokuwa wamefunikiwa kimafanikio katika macho ya mashabiki wa muziki. 2017 ni mwaka tutakaoshuhudia mengi makubwa kwenye muziki huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni