RAPA Joh Makini ni miongoni mwa wasanii wachache waliodumu kwa muda mrefu kwenye muziki wa hip hop kwa hapa Bongo huku wakiendelea kufanya vizuri kwa kipindi chote.
Kuanzia kipindi cha River Camp Soldiers mpaka sasa Weusi, bado Joh Makini anaonesha uwezo wake wa kuandika, kurap na kucheza na jukwaa pindi anapokua kwenye ‘show ‘zake. Ubora wa kazi zake ndo umemfikisha hapa alipo kwa sasa, nasema hivi kwa sababu si mtu wa kutumia ‘skendo’ au matukio kwa ajili ya kuutangaza au kuupa nguvu muziki wake.
Kama tunavyo fahamu muziki wa hip hop na wa RnB una ukaribu mkubwa sana, hivyo si ajabu kwa wasanii wa hip hop au RnB wakifanya kazi pamoja. Nilipokaa na kufikiri kwa akili ya kawaida tu, niligundua kuwa Joh Makini amekuwa chaguo namba moja kwa wasanii wa RnB kwa siku za hivi karibuni, hasa pale wanapotaka kufanya kazi na msanii wa hip hop.
Na kwa sababu hiyo wasanii wengi wa RnB wamejikuta wakiingia kwenye orodha ya kufanya kazi na Joh Makini, leo kupitia Bongo Count Down nakuletea orodha ya wasanii hao.
1.Rama Dee
Rama Dee ni mmoja kati ya wasanii ambao hutoweza kuacha kumtaja kama mtu aliyetoka mbali na mziki wa RnB kwa hapa bongo. Ngoma aliyofanya na Joh Makini ilikwenda kwa jina la ‘Sina Muda’, ni ya kitambo kidogo. Mwaka 2014 Rama Dee alishinda tuzo ya KTMA ya wimbo bora wa RnB, Kwa wimbo wake wa ‘Kuwa na Subira’ aliowapa shavu kundi la Mapacha.
2.Ben Pol
Mkali huyu wa RnB zaidi ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuimba, pia ni mwandishi mzuri wa nyimbo, mwaka 2013 alishinda tuzo ya KTMA kama mtunzi bora wa mashairi ya Bongo Fleva. Aliamua kumshirikisha Joh Makini kwenye ngoma yake ya ‘Unanichora’ uliyopikwa na prodyuza Fundi Samweli.Kolabo hii lilisumbua sana kwenye vituo vya redio na runinga kutokana na ubora wa video yake, hadi leo ni mingoni mwa ngoma za Ben Pol anazoweza kujivunia.
3. Jux
Kwa mara ya kwanza Jux na Joh Makini walishirikishwa na Nick wa Pili kwenye ngoma ya Safari ambayo ilijumuisha wakali kibao kama Vanessa Mdee G Nak, Nahrel na Aika (Navy Kenzo). Baada ya hapo Jux aliamua kumpa shavu Joh Makini kwenye ngoma yake ya ‘Looking for You’, iliyopikwa na Nahrel kwenye studio za The Industry. Ngoma hii ilifanya vizuri sana hapa Bongo na hata kwenye vituo vya runinga vya kimataifa. Mwaka 2014 Jux alishinda tuzo ya KTMA kupitia ngoma yake ya ‘Sisikii’.
4.Damian Soul
Wameshafanya kazi mbili pamoja, zote zikiwa za Damian Soul, kazi ya kwanza iliyokwenda kwa jina la ‘Ni Penzi’, ambayo ilifanya vizuri sana na kumtambulisha zaidi Damian Soul kwenye muziki. Ngoma hiyo ilitajwa na KTMA kuwania tuzo ya wimbo bora wa RnB kwa mwaka 2014, ingawa haikushinda.
Damian Soul aliamua kufanya kazi nyingine na Joh Makini iliyofahamika kama ‘Baraka’, kwa bahati mbaya kazi hii haikupata mzunguko mzuri kwenye vituo vya redio ila ilikuwa ni kazi nzuri kutoka kwenye mikono ya Pancho Latino wa B’ Hits.
5.Q Jay
Ni jina lilopotea kwenye muziki wa Bongo Fleva kwa muda mrefu sasa, alikuwa ni mingoni mwa wasanii waliyounda kundi la Wakali Kwanza akishirikiana na Josline na Makamua. Kuna kipindi alitangaza kuacha muziki wa kidunia na kuanza kufanya muziki wa injili, huenda ni moja ya sababu ya yeye kutosikika kwa sasa. Q Jay alishafanya kazi na Joh Makini kwa miaka ya nyuma ambayo mpaka sasa inaishi kwenye muziki wa RnB. ‘Sintorudi’ ndo jina la ngoma hiyo.
6. Belle 9
Ni mkali wa RnB anayefananishwa na ule usemi wa nabii hakubaliki nyumbani kwao, licha ya kutoa ‘hits’ kibao hajawahi kupewa tuzo kutoka hapa Bongo kama kuheshimu kile anachofanya. Lakini habari nzuri ni kwamba washabiki wake waishio Berlin Ujerumani walimua kumpa tuzo kwa kutambua ubora wa kazi zake, tuachane na hilo. Alimshirikisha Joh Makini kwenye ngoma yake ya ‘Vitamin Music’ iliyopikwa na produyza Mona Gangstar. Kufanya vizuri kwa ngoma hiyo ndo kulipelekea Belle 9 kufungua kampuni kwa ajili ya kusimamia kazi zake na kuipa jina la Vitamin Music.
7. TID
Mwenyewe anajiita ‘mzee kigogo’ ameshafanya kazi na wakali wengi wa hip hop hapa bongo akiwemo Prof Jay, Fid Q na Jay Moe kwa kipindi cha nyuma. Aliona sio mbaya kama Joh Makini na yeye akiingia katika orodha yake, ndipo alipompa shavu kwenye ngoma yake ya Confidence ambayo ilitoka mwanzoni mwaka jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni