Rehema Chalamila, how I wish arudi tena kwenye chati kama zamani. Ray
C – kama unavyomjua zaidi, amepitia mapito mengi, na tena yaliyojaa
njia yenye mbigili ibakishayo maumivu mguuni.
Miaka minne iliyopita, kwa hali aliyokuwa nayo, kila mtu alimkatia
tamaa kuwa ndio basi tena ameshatumbukia kwenye shimo waliloshindwa
kutoka vijana wengi. Matumizi ya madawa ya kulevya yalimuongezea jina la
uteja lililolifunika jina lake la utani ‘kiuno bila mfupa.’ Rehema,
msichana mrembo aliyekuwa ndoto ya wanaume wengi, akapoteza thamani
yake.
Jina lake likapotea kwenye ramani ya muziki na akawa mtu wa kuonewa
huruma. Na kwa jinsi madawa ya kulevya yalivyo, humnyong’onyeza
mtumiaji, humpunguzia utimamu wake kiakili, humpa utegemezi unaotesa
yasipotumiwa na ikawa wakati mwingi Rehema akawa wa kukutwa amezima!
Maskini wa Mungu Ray C akaingia kwenye dimbwi la maji ya moto ya uteja,
nani wa kumuokoa?
Kwa alama aliyoiweka kwenye muziki wa Tanzania kwa nyimbo kibao
zilizofanya vizuri, Ray C akapata msaada kutoka kwa mtu mwenye cheo
kikubwa zaidi nchini, Rais Jakaya Kikwete. Alijitolea kumpeleka rehab,
kumsadia kwa hali na mali hadi hali yake ikarudi kwenye mstari – walau
kwa muda huo. Aliingia kwenye mpango wa kutumia methadone aliodumu nao
kwa takriban miaka mitatu.
Katika kipindi hicho, Ray C akageuka kuwa kinara wa vita dhidi ya
matumizi ya madawa ya kulevya. Alianzisha pia taasisi yake, The Ray C
Foundation kwaajili ya kampeni za kukemea ubwiaji unga. Katika kipindi
hicho, Rehema, alijaribu tena kurejea kwenye muziki kwa kuachia wimbo
mmoja ‘Mshum Mshum’, ambao hata hivyo haukufanikiwa kumrudisha pale
alipokuwa ameishia.
Haikuwa rahisi kuishinda vita hiyo na mwaka huu alionekana kuweka
silaha chini kwa kudaiwa kurejea tena kwenye matumizi ya madawa hayo.
Video iliyosambaa mtandaoni akionekana akiwa kwenye mvurugano wa akili,
akilia na kutaka kujichoma kisu, ilirejesha tena hofu kwa wapenzi wa
muziki kuwa amerudi kwenye jela ya uteja.
RAY C ANARUDI
Peleka mbele hadi wiki moja iliyopita, Ray C anaonekana kupata chaji
ya muziki inayompeleka hadi kwenye studio za kisasa za Wanene
Entertainment. Kwanza nimefurahi kuona amebadilika mno kutoka yule
msichana aliyenenepa hadi kuupoteza utambulisho wake. Amerudisha umbo
lake la zamani linalompa matumaini ya kulikomboa jina la jukwaani –
kiuno bila mfupa.
Uhakika nimeupata kwenye video alizoziweka Instagram zikimuonesha
akiwa kwenye mazoezi makali ya kucheza huku kiuno chake kikifuata vyema
maagizo kinayopewa. Huu unaweza kuwa urejeo wenye nguvu zaidi wa
muimbaji huyu na namuomba Mungu amsaidie kukaa tena kwenye nafasi yake.
Muziki wa Tanzania unamhitaji Ray C hasa kwakuwa kuna upungufu wa
wasanii wakubwa wa kike. Inanipa moyo kuona mahaba yake ya muziki
yamerudi kwa kasi ya ajabu. Napata amani nikimuona anavyofurahia
mchakato wa kutengeneza nyimbo mpya. Nafarijika kuona kuwa amezungukwa
na watu wanaotaka arudi kwenye chati.
Atakachohitaji baada ya hapo ni kuungwa mkono na vituo vyote vya
redio nchini na pia mashabiki wakitimiza wajibu wao. Yapaswa kukumbuka
kuwa muziki pekee ndio unaweza kuwa mkombozi kwake na unaoweza kumpa
nafasi ya pili – nafasi ya kung’ara tena.
Naamini anarekodi nyimbo nyingi na katika hizo lazima kutakuwa na
nyimbo kubwa. Pamoja na matatizo yote aliyoyapita, sijawahi kuwa na
shaka na kipaji chake. Nasubiri kwa hamu kusikia kile alichotuandalia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni