burudan

https://share.bannersnack.com/bdtkqutzy/

31 Okt 2016

Huu unaweza kuwa ujio mzito na mpya wa Ray C kimuziki

Rehema Chalamila, how I wish arudi tena kwenye chati kama zamani. Ray C – kama unavyomjua zaidi, amepitia mapito mengi, na tena yaliyojaa njia yenye mbigili ibakishayo maumivu mguuni.
Miaka minne iliyopita, kwa hali aliyokuwa nayo, kila mtu alimkatia tamaa kuwa ndio basi tena ameshatumbukia kwenye shimo waliloshindwa kutoka vijana wengi. Matumizi ya madawa ya kulevya yalimuongezea jina la uteja lililolifunika jina lake la utani ‘kiuno bila mfupa.’ Rehema, msichana mrembo aliyekuwa ndoto ya wanaume wengi, akapoteza thamani yake.
Jina lake likapotea kwenye ramani ya muziki na akawa mtu wa kuonewa huruma. Na kwa jinsi madawa ya kulevya yalivyo, humnyong’onyeza mtumiaji, humpunguzia utimamu wake kiakili, humpa utegemezi unaotesa yasipotumiwa na ikawa wakati mwingi Rehema akawa wa kukutwa amezima! Maskini wa Mungu Ray C akaingia kwenye dimbwi la maji ya moto ya uteja, nani wa kumuokoa?
Kwa alama aliyoiweka kwenye muziki wa Tanzania kwa nyimbo kibao zilizofanya vizuri, Ray C akapata msaada kutoka kwa mtu mwenye cheo kikubwa zaidi nchini, Rais Jakaya Kikwete. Alijitolea kumpeleka rehab, kumsadia kwa hali na mali hadi hali yake ikarudi kwenye mstari – walau kwa muda huo. Aliingia kwenye mpango wa kutumia methadone aliodumu nao kwa takriban miaka mitatu.
Katika kipindi hicho, Ray C akageuka kuwa kinara wa vita dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya. Alianzisha pia taasisi yake, The Ray C Foundation kwaajili ya kampeni za kukemea ubwiaji unga. Katika kipindi hicho, Rehema, alijaribu tena kurejea kwenye muziki kwa kuachia wimbo mmoja ‘Mshum Mshum’, ambao hata hivyo haukufanikiwa kumrudisha pale alipokuwa ameishia.
Haikuwa rahisi kuishinda vita hiyo na mwaka huu alionekana kuweka silaha chini kwa kudaiwa kurejea tena kwenye matumizi ya madawa hayo. Video iliyosambaa mtandaoni akionekana akiwa kwenye mvurugano wa akili, akilia na kutaka kujichoma kisu, ilirejesha tena hofu kwa wapenzi wa muziki kuwa amerudi kwenye jela ya uteja.
RAY C ANARUDI
Peleka mbele hadi wiki moja iliyopita, Ray C anaonekana kupata chaji ya muziki inayompeleka hadi kwenye studio za kisasa za Wanene Entertainment. Kwanza nimefurahi kuona amebadilika mno kutoka yule msichana aliyenenepa hadi kuupoteza utambulisho wake. Amerudisha umbo lake la zamani linalompa matumaini ya kulikomboa jina la jukwaani – kiuno bila mfupa.
14717437_193840194391121_4773183368646885376_n
Uhakika nimeupata kwenye video alizoziweka Instagram zikimuonesha akiwa kwenye mazoezi makali ya kucheza huku kiuno chake kikifuata vyema maagizo kinayopewa. Huu unaweza kuwa urejeo wenye nguvu zaidi wa muimbaji huyu na namuomba Mungu amsaidie kukaa tena kwenye nafasi yake.
14676582_1467445509939009_6886310319115730944_n
Kutoka Kushoto: Anna Peter wa East Africa Radio, Ray C na Mamy Baby wa Clouds FM
Muziki wa Tanzania unamhitaji Ray C hasa kwakuwa kuna upungufu wa wasanii wakubwa wa kike. Inanipa moyo kuona mahaba yake ya muziki yamerudi kwa kasi ya ajabu. Napata amani nikimuona anavyofurahia mchakato wa kutengeneza nyimbo mpya. Nafarijika kuona kuwa amezungukwa na watu wanaotaka arudi kwenye chati.
Atakachohitaji baada ya hapo ni kuungwa mkono na vituo vyote vya redio nchini na pia mashabiki wakitimiza wajibu wao. Yapaswa kukumbuka kuwa muziki pekee ndio unaweza kuwa mkombozi kwake na unaoweza kumpa nafasi ya pili – nafasi ya kung’ara tena.
Naamini anarekodi nyimbo nyingi na katika hizo lazima kutakuwa na nyimbo kubwa. Pamoja na matatizo yote aliyoyapita, sijawahi kuwa na shaka na kipaji chake. Nasubiri kwa hamu kusikia kile alichotuandalia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni