burudan

https://share.bannersnack.com/bdtkqutzy/

6 Mei 2017

HASARA ROHO YA DARASSA ITAENDELEZA UTEMI ULIOACHWA NA MUZIKI?


Kutoa ngoma kubwa huchanganya uchungu na utamu kwa wakati mmoja. Utamu ni show kumiminika kuanzia Jumatatu mpaka Jumatatu nyingine – hadi utazikimbia. Uchungu ni pressure na matarajio ya ngoma inayofuata – hapo pagumu na wasanii wengi pamewashinda.

Lakini mtu aliyekuwa na deni kubwa kuliko wote ni Darassa. Wimbo wake Muziki ulikuwa anthem ya mwaka 2016 na umemfanya kutoka kuwa rapper aliyekuwa akihangaika kutafuta tobo hadi msanii keki ya moto anayetafutwa kwa show kila kona. Deni lake lilikuwa kubwa – anatokaje baada ya Muziki?

Siku ya kulipa deni haichelewi, Darassa amebisha tena hodi na wimbo mpya mkonini – Hasara Roho. Ni jina unique, lakini limewahi kutumiwa pia na Naylee na ambalo licha ya kuwa ni la Kiswahili, bado sijawahi kuelewa maana yake. Wimbo huu ukiusikiliza, haraka tu, ni rahisi kupata ladha ya kaka yake, Muziki.

Ufanano wa nyimbo hizi mbili upo kwenye mtindo aliotumia, mituo katika mashairi yake, lakini ujenzi wa mashairi yenye madongo kama ‘unataka kucheza wewe na ushike filimbi’ yenye muktadha ule ule kama yaliyomo kwenye Muziki mfano : Unataka kukimbia na hauna break, what do you expect!’

Kwa ufupi kimashairi na mtindo, Hasara Roho ni kama muendelezo wa Muziki lakini ulioboreshwa zaidi. Hapa, hata hivyo, wazungu wangesema ‘ameplay safe.’ Kutohama kwake sana kwenye Muziki kunaifanya ‘transition’ ya kutoka kwenye anthem ambayo haikuwa rahisi kuipiku, kukopa vionjo vyake kuhama na kuendelea na safari nyingine. Kwenye Hasara Roho, Darassa bado anaishi kwenye ulimwengu wenye mafanikio wa Muziki. Kwahiyo, inakuwa nafuu kwake kuendelea kuchezea kwenye utawala wa wimbo huo uliopita na hivyo kuepuka uwezakano wa kukaribisha kauli za ‘ameshindwa kuifunika Muziki.’

Lakini pia licha ya ufanano huo, kwa muundo wa midundo kwenye Hasara Roho, Darassa amefanikiwa. Ameendelea kutumia midundo ya aina yake yenye Uafrika mwingi kama vile marimba – silaha itakayoufanya wimbo huu nao uende mbali. Kikubwa kuliko vyote, kwenye wimbo huu, Darassa amethibitisha kuwa hakamatiki kwenye uandishi wa mashairi ya shombo. Hakuna shaka, Hasara Roho itatengeneza misemo mingi mtaani kama ambavyo Muziki ilifanya.

Muhimu pia ni kuwa Darassa ameifahamu siri ya kutengeneza nyimbo ‘catchy’ ambazo ukizisikiliza tu unajikuta zinakubeba. Na pia ametengeneza mtindo wake mwenyewe ulio tofauti kabisa na nyimbo zingine za Bongo. Huu ni mtindo ambao aliuanza kwenye Too Much.

Ninaamini kuwa wimbo huu utafanya vizuri pia na hivyo kumpa Darassa muda mwingine mrefu wa kuzikusanya hela zake kupitia shows na deals zingine. Sina wasiwasi na ubora wa video yake ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa. Naamini nayo itavutia views nyingi kama ilivyofanya Muziki ambayo hadi sasa Youtube ina views milioni 7.5.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni